JUKWAA HURU LA VIJANA TANZANIA.

Ndugu zangu, katika historia tunaelezwa kuwa kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwa Chama cha Tanganyika African National Union yaani TANU mwaka 1954 mbinu nzuri ambayo imekuwa ikitumiwa katika kujiweka imara kisiasa na kuendesha mikakati kwa uthabiti, ni kupitia jumuia zake za wanawake, vijana na wazazi.

Ndugu zangu, historia ya shughuli za kisiasa nchini, zinaonesha kuwa jumuia za chama kwa nafasi zao zina mchango mkubwa sana katika kuleta maendeleo ya kisiasa kabla na baada ya uhuru.

Kwa mfano, katika zama za harakati za kugombea uhuru nchini, tunaambiwa na wazee wetu kuwa Umoja wa Kinamama wa TANU wakiongozwa na Bibi Titi Mohamed walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha uhuru wa Tanganyika, ambapo aliwaunganisha kinamama mbalimbali vikiwemo vikundi vya wapika pombe wa Dar es Salaam.

Kulikuwa na Jumuia ya Vijana ya Chama cha TANU na ASP na leo hii sehemu kubwa ya viongozi waliopo madarakani nchini, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete walikuwa wameiva kisiasa kupitia jumuia hiyo.

Ndugu zangu, enzi hizo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na wenzake walitengeneza mtandao bora wa kuibua, kulea na kukuza vipaji vya uongozi vijana na hatimaye kupatikana viongozi hao akiwemo William Lukuvi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita na hata Seif Khatibu, nikiwataja kwa uchache.

Kupitia Umoja wa Vijana wa CCM (zamani TANU), wafanyakazi walijipanga kwa kuwa na maandalizi ya vijana katika hatua zifuatazo, Malezi ya awali ambayo yalianzia chipukizi ambapo vijana wadogo hadi kwenye umri unaokomea elimu ya msingi walijihusisha na mambo mbalimbali yahusuyo chama chao cha TANU baadaye CCM, propaganda na wajibu wao wa jumla.

Kulikuwa na mafunzo maalum ya chipukizi ambayo yalianzia katika ngazi ya chekechea, na katika mafunzo ya awali yalisaidia mno kuwajenga vijana kuwa wanachama watiifu wanaokielewa vyema chama, huku wakifundishwa kuwa ‘rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.’

Ndugu zangu, huo ulikuwa msingi wa kwanza kabisa wa kuwajenga vijana. Vijana hao waliendelea kujengwa katika ngazi mbalimbali kama vile kupitia Jeshi la Kujenga Taifa kwa wale waliokuwa wamemaliza kidato cha sita au kozi, hatimaye chama kilifika mahali kijana anapofikia umri wa mtu mzima anakuwa amejitosheleza katika kila namna kama vile uelewa wa maudhui ya chama, imani, propaganda, ulinzi na anakuwa kada mzuri wa kutumikia chama chake na taifa kwa uaminifu mkubwa.

Ndugu zangu aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM ambaye sasa ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Emmanuel Nchimbi, aliwahi kuhojiwa na chombo kimoja cha habari akasema msingi wake wa kufahamu na kupenda siasa ulianza alipokuwa kijana chipukizi akiwa mtoto wa kada wa CCM katika Chuo cha CCM Kivukoni, akimkumbuka vyema mwalimu wake wa chipukizi, Philip Mangula ambaye baadaye alikuwa Katibu Mkuu wa CCM.

Viongozi kama Nchimbi walioandaliwa na chama tangu wakiwa wadogo wapo wengi hali iliyomfanya kupanda na kuchaguliwa kuwa mbunge mwaka 2005 kisha akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, kisha Naibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa lakini awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda.

Ndugu zangu, nimemtumia Nchimbi kama mfano wakilishi, kuonesha matunda ya mafanikio yake kisiasa yanatokana na maandalizi yaliyoanzia katika ngazi ya chipukizi, kwani hata baada ya kuhitimu shule, aliendelea kuwa kada mahiri wa CCM alipokuwa katika kilichokuwa Chuo cha Maendeleo ya Uongozi (IDM)- Mzumbe (sasa Chuo Kikuu cha Mzumbe). Sasa anatumikia CCM katika ngazi ya taifa akiwa amesheheni uzoefu wa kutosha.

Ndugu zangu, nia yangu ni kuonesha kuwa vijana wakiandaliwa katika chama kuanzia wakiwa wadogo, siyo CCM bali katika kila chama, wanakuwa wapenda nchi na wazalendo, kwa mfano wapo akina Amosi Makalla, Dk. Mathayo David na wengineo wa CCM, au Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia, Joseph Selasini wa Chadema, Zitto Kabwe ambaye ukizungumza naye anakuambia alianza kupenda siasa akiwa sekondari.

Ndugu zangu namkumbuka sana Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba katika Mkutano wa Uchumi Duniani, uliofanyika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, alifafanua kwamba namna bora ya kupata viongozi kitaifa ni kuwa na utaratibu wa kuwatambua mapema vijana wenye vipaji vya uongozi na kuwaandaa.

Ndugu zangu, hili kwangu mimi naona kama lilikuwa angalizo kutoka kwa mzee Jaji Warioba, na linasaidia kufungua macho juu ya nafasi ya vijana katika jumuiya zao ndani ya vyama vya siasa, (nazungumza haya bila kujali itikadi zao), ili kuzalisha viongozi kwa manufaa ya taifa la kesho.

Uzuri ni kuwa hata viongozi wengi wa upinzani wametokea CCM kwa hiyo wanajua kuwa ule mchakato ulioshikana tangu ngazi ya chipukizi hadi taifa na kuandaa viongozi umelegalega na sasa kuna haja ya jumuiya za vijana kuangalia namna gani zinaweza kurudisha mtiririko bora wa kipindi kilichopita kwa kuwa na mtandao bora na wenye mafunzo imara ya chipukizi na hatimaye kwa makada kamili katika vyama vyao ili watumikie taifa kwa uaminifu.

Ndugu zangu, ikiwa vyama vitafanya hivyo itasaidia kujenga vyema uzalishaji wa viongozi bora wa kesho na siyo bora viongozi. Kila chama kina uwezo wa kujenga mtandao bora wa makada wa kweli na wenye uzalendo wa uhakika kukitetea chama chao japo viongozi wa kisiasa na kiutawala katika chama na serikali.

Kila chama kikumbuke kuwa kinapotenga nafasi ya wabunge na madiwani wa viti maalum kwa vijana, uteuzi usiwe katika misingi ya kujaza nafasi bali anayeteuliwa ajaze nafasi awe na sifa na maadili yanayotakiwa katika uongozi na uzalendo iwe sifa ya nyongeza. karibuni katika chombo hiki huru chenye kulenga kukomboa vijana kwa mijadala itakayowapa maarifa na ujuzi wa kuweza kuenenda katika mienendo na maadili mema.hatufungamani na ilani wala itaikadi ya dini,kabila,jinsia au chama chochote haopa ni mahala pa kuleta na kuchambua fikra za vijana juu ya ustawi wa taifa letu.tujadili kwa heshima na

uvum ilivu wa hoja zozote isipokuwa matusi